Thursday 7 May 2015

JUA FAIDA YA ZAO LA MUHOGO KIUCHUMI

Zao la muhogo kwa wananchi walio wengi linachukuliwa kama la kinga dhidi ya njaa. Miaka ya hivi karibuni kumezuka teknolojia nzuri ya kufanya zao la muhogo litumike kwa usafi zaidi na hata kuwa zao la biashara zaidi jambo ambalo litawafanya wakulima wa Tanzania kuwafikia
Zao la muhogo
wakulima wa Afrika Magharibi ambao wameanza kusindika zao la muhogo kwa muda mrefu na kunufaika kiuchumi.
Utafiti uliofanyika nchini Italia kuhusiana na zao hilo unaonyesha kuwa muhogo unaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali zaidi ya 300 yakiwemo unga wa muhogo, tambi, biskuti, mafuta ya lishe, keki, sabuni ya
unga, kuni, mboga, pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Maofisa ugani wakieneza elimu ya kisasa ya kusindika muhogo katika maeneo mengi nchini miaka kumi ijayo, zao la muhogo litakuwa ni zao kubwa na lenye heshima katika kuinua uchumi na kipato cha mkulima kwa kulifanya kuwa zao la chakula na biashara.

Takwimu kutoka Idara ya Kilimo wilayani Songea mkoani Ruvuma zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la muhogo umefikia wastani wa tani 30,000 tu kwa mwaka uzalishaji ambao bado upo chini kutokana na wakulima wengi kukosa utaalamu wa kulisindika zao hilo.
Taarifa ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.
Hii ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.
Aidha, katika baadhi ya maeneo zao hilo hutumika kama chakula cha mifugo na sehemu kidogo ya zao hilo husafirishwa nje ya nchi.
Nchi ya Brazil hivi sasa imesonga mbele katika uchumi na teknolojia kwa kuwa tayari imeanza kutengeneza magari yanayotumia nishati mbadala inayotokana na mimea kama muhogo.
Zao la muhogo lina mizizi inayotoa wanga, unga na nishati wakati majani ya mhogo ni chakula kizuri chenye vitamini, protini na madini ya chuma ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu.
Utafiti unaonyesha kuwa Tanzania ni moja ya nchi wazalishaji wakubwa wa muhogo duniani ambapo katika bara la Afrika, Tanzania inachukua nafasi ya nne baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC.
Kutokana na hali hiyo Tanzania ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa zao la muhogo hata kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kutokana na kuwa na utajiri wa ardhi kubwa yenye rutuba.
Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania inazalisha muhogo kwa wastani wa tani mbili tu kwa mwaka kwa hekta na wastani wa bara la Afrika ni tani 3.3 kwa mwaka, wastani wa Nigeria ni tani 4.7 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment